Februari 21 majira ya saa mbili usiku watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha aina ya SMG/SAR walivamia katika kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu huko eneo la Jaribu Mpakani kata ya Majawa, Kibiti na kuuwa watu watatu, ambao ni Ofisa upelelezi wa Kibiti, mfanyakazi wa Halmashauri na mlinzi wa kituo cha kukagulia mazao ya mali asili kata ya Jaribu Mpakani.
Kufuatia tukio hilo, Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Lameck Nchemba amefika eneo la tukio ambapo ameeleza kusikitishwa na tukio hilo.
Waziri Nchemba amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuwataja wahusika wa tukio hilo ambalo mazingira yake yanaonyesha mpango huo unafahamika na baadhi ya wananchi hao.
Amesema Serikali haiwezi kufumbia macho vitendo hivyo vya mauaji ya watu kama Mende huku shughuli nyingine zikiendelea.
“Tutawalinda Watanzania wasiokuwa na hatia kwa gharama yoyote ile, na tutapambana na wale wanaouwa kwa gharama yoyote ile…” – amesisitiza Waziri Nchemba