Bingwa wa zamani wamasumbwi ya uzito wa Welterweight, Floyd Mayweather ameingia kwenye chumba cha maandalizi cha bondia Manny Pacquiao ikiwa zimebaki dakika chache bondia huyo Mfilipino apande ulingoni.

Pacquiao anaingia ulingoni kupambana rafiki wa Mayweather, Adrien Broner katika pambano litakaloshuhudiwa dakika chache zijazo na mamilioni ya watu duniani, likirushwa moja kwa moja kutoka Las Vegas nchini Marekani.

Mayweather ambaye alistaafu akiwa hajapoteza pambano hata moja kati ya mapambano yake 50, alimkumbatia Pacquiao ambaye alikuwa tayari amevaa gloves.

 

Vivyo hivyo, alipita kwenye chumba cha rafiki yake Broner na kumtakia kila la kheri.

Hatua hiyo ya Mayweather imezidi kuchochea kuni za uwezekano wa kuwepo pamban la marudiano kati ya mabondia hao mapema mwaka huu, dalili ambazo zilikuwa zimeanza kuyoyoma licha ya ahadi waliyoitoa Septemba mwaka jana walipokutana Tokyo, Japan.

Wababe hao walipigana Mei 2015, ambapo Mayweather alishinda kwa matokeo ya majaji baada ya raundi 12 (Unanimous decision).

Katika pambano la leo, Pacquiao anatetea ushindi wake wa ubingwa wa dunia wa mkanda wa Chama Cha Ngumi Duniani (WBA), alioupata mwaka jana baada ya kumpiga kwa KO bondia Lucas Matthysse.

Hili ni pambano lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 40, na anahitaji ushindi muhimu leo ili afanikishe ndoto yake ya kupata pambano la marudiano na Mayweather.

Mayweather atakuwa mmoja kati ya watu watakaotoa maoni yao kama wachambuzi wakiwa karibu na ulingo kupitia kituo cha runinga cha ShowTime.

Kaa hapa Dar24 utapata matokeo ya pambano hilo punde.

Kauli ya CAG yawakuna CCM, 'Acheni propaganda'
Simba yaufyata kwa AS Vita, yapokea kipigo cha 'Mbwa koko'