Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kuwa uchumi wa Tanzania unazidi kuporomoka kadri siku zinavyozidi kusonga mbele huku akiitahadharisha Serikali kuchukua hatua stahiki za kunusuru hali hiyo.
Ameyasema hayo mapema hii leo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa ni vyema Serikali ikabadili mfumo wa uendeshaji hasa katika sekta ya uchumi.
“Uchumi wa Tanzania unazidi kuporomoka kila kukicha, viongozi walioko Serikalini wanawandanganya wananchi kuwa uchumi unapanda kumbe si kweli, mfano mzuri ni bandari ya Dar es salaam imekufa,”amesema Mbowe
Hata hivyo, ameongeza kuwa taasisi nyingi za binafsi zinafunga biashara zao kwa sababu ya uendeshaji mbovu wa Serikali hasa katika ukusanyaji wa kodi hali ambayo inasababisha wawekezaji wengi kuondoka nchini.