Mbunge wa Kawe, Halima Mdee amezungumzia mtazamo na maswali yanayoulizwa kuhusu kutoonekana kwa viongozi wa kitaifa wa Chadema, katika mazishi ya watu waliofariki kutokana na ajali ya kivuko cha MV Nyerere mkoani Mwanza.

Mdee ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa chama hicho waliohudhuria uzinduzi wa Sera za chama hicho wiki hii jijini Dar es Salaam, alikanusha taarifa za kutohudhuria kwa viongozi wa kitaifa wa chama hicho kwenye mazishi hayo akieleza kuwa huenda tafsiri ya viongozi hao ndio tatizo.

“Inategemea tafsri yako ya kiongozi wa kitaifa. Kwa mfano, sisi Chadema tuna ngazi ya Kitaifa kwa mantiki kwamba uongozi wa Taifa ambapo kuna Mwenyekiti wa Taifa. Lakini pia tuna viongozi wa kanda, hao viongozi wa kanda ni wajumbe wa Kamati Kuu, maana yake ni viongozi wa kitaifa,” Mdee aliiambia Dar24.

“Sisi Chadema tuna wabunge ambao nao ni viongozi wa kitaifa. Kwenye ule msiba walihudhuria viongozi wa Kanda ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu, alihudhuria mbunge. Sasa kama mnatoa tafsiri ya kuhudhuria msiba kwa mtu aliyepewa nafasi ya kuzungumza pale kwenye TV live, sasa hicho ni kitu kingine,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Mdee alieleza kuwa hatua zilizochukuliwa dhidi ya viongozi ikiwa ni pamoja na kuvunja Bodi ya Wakala wa Umeme na Ufundi (Temesa), hazikutakiwa kuishia hapo, bali pia mawazili husika walipaswa kuwajibika.

Watu zaidi ya 200 walifariki dunia kutokana na ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere wiki iliyopita. Mazishi yalifanyika Jumapili na kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa wa Serikali, wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Septemba 26, 2018
Lowassa awajibu wanaomshauri kustaafu siasa