Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wafuasi wa ngome ya upinzani ya Kenya ya National Super Alliance (NASA) wamefanikiwa kugundua mizinga ya nyuki iliyokuwa imetegwa kwenywe uwanja wa Uhuru Park, walipopanga kufanya tukio la kumuapisha Raila Odinga kuwa Rais.
Picha za video zilizooneshwa na kituo cha runinga cha KTN nchini humo zimeonesha wafuasi hao wa Raila ambao wameanza kumiminika katika uwanja huo tangu alfajiri wakichoma baadhi ya mizinga iliyokuwa imefichwa nyuma ya miti, huku wakiendelea kutafuta kama kuna mizinga mingine.
Leo, jiji la Nairobi na Kenya kwa ujumla itashuhudia kitakachotokea wakati wafuasi wa NASA wanapojaribu kufanya tukio la kumuapisha Raila katika uwanja huo ambao tayari jeshi la polisi limeshakataza watu kukusanyika hapo.
Many left puzzled as bee hives are found at Uhuru Park#NASASwearingIn pic.twitter.com/2mohFo9v3k
— KTN News (@KTNNews) January 30, 2018
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, mamia ya mabasi yameendelea kusafirisha umati wa wafuasi wa NASA kutoka mikoa mbalimbali ya karibu kuelekea Nairobi.
Imeripotiwa kuwa mabasi manne yaliyobeba wafuasi hao kutoka maeneo ya nje ya Nairobi yamekamatwa na kuzuiliwa kutokana na makosa ya usalama barabarani.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, NASA walibadili uamuzi wao wa kumuapisha Raila kuwa Rais wa Watu na kutangaza kuwa wamemuandaa Jaji kwa ajili ya kumuapisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, nafasi ambayo inashikiliwa na Rais Uhuru Kenyatta aliyeshinda uchaguzi wa marudio na kuapishwa.
Hakuna anayefahamu kitakachotokea katika tukio hili la leo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wengi wameeleza kuwa kwa hali ilivyo haitabiriki hivyo ni ‘kusubiri kushuhudia’.