Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika ameingilia kati suala zima la Wakuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya kuchukua sheria mkononi na kuwaachisha kazi baadhi ya watumishi wa Serikali wakati wao sio waajiri wao.
Hivyo ameomba aletewe watumishi wote waliofukuzwa kazi na wakuu wa mkoa au wakuu wa wilaya ili aweze kushughulikia suala hilo mara moja akifuata taratibu za kiutumishi zinazompa madaraka mwajiri peke yake kuadhibu watumishi wake aidha kwa kuwafuta kazi au kuwasimamisha kwa muda.
”Yule aliyekuajiri wewe ndio mwenye madaraka ya kukufukuza kwahiyo utaona kwamba mara nyingi wakigundua kwamba kuna makosa wanamsimamisha wakati wanasubiri yule mwenye madaraka ya ajira achukue hatua za mwisho, naliomba bunge hili kama kuna mahala mtumishi amefukuzwa na mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya wakati yeye si aliyemwajiri niletewe suala hilo nitalishughulikia mara moja kwa sababu kwa taratibu zetu za kiutumsihi yule aliyekuajiri ndiyo anayekuadhibu ndiye anayekufukuza”. Amesema Mkuchika.
Hivyo ametaka viongozi kutumia vyema madaraka yao kama ambavyo walifunzwa pindi walipoteuliwa.