Hali ya hewa nchini Marekani imechafukwa tena baada ya tukio baya la polisi kumkamata kijana mmoja Mmarekani Mweusi usiku wa kuamkia jana na kisha kumpiga risasi takribani sita kifuani na mgogoni.

Video iliyorekodiwa na raia mmoja msamalia mwema ilionesha polisi wawili wa kizungu wakimkimbiza kijana huyo aliyetambulika kwa jina la Alton Sterling. Polisi walichukua hatua hiyo baada ya kupokea simu kutoka kwa mtu asiyejulikana majira ya saa sita na nusu usiku wa kuamkia jana, kuwa kuna mtu anawatishia watu kwa bunduki nje ya duka moja huko Baton Rouge, Louisiana.

Katika kipande hicho cha video, polisi walimkamata Sterling na kumbana kisha mmoja akammiminia risasi kadhaa kifuani baada ya kusikika akisema kwa sauti ‘ana bunduki’.

Mmiliki wa duka hilo ambaye alifanikiwa kuchukua vipande vingine vya video vya tukio hilo ameeleza kuwa kijana huyo hakuwa ameshikilia bunduki wala mikono yake haikuelekea mfukoni wakati huo.

Jeshi la Polisi la Baton Rouge limeeleza kuwa polisi wawili waliohusika katika tukio hilo, Blane Salamoni na Howie Lake wamepewa likizo ya kiutawala.

Watu wengi wakiwemo watu maarufu weusi nchini humo wameonesha kupinga kwa nguvu hatua hiyo kupitia mitandao ya kijamii na huenda maandamano makubwa yakaandaliwa mitaani.

Dk. Shein amtaka Maalim Seif kusahau ‘Serikali ya Mpito’, Seif adai yuko tayari kukamatwa
Lionel Messi afungwa jela miezi 21 kwa ufisadi