Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina amesema kuwa Serikali imejipanga kuondoa kero za upatikanaji wa vyeti vya tathmini ya athari ya mazingira kwani imeonekana kuwa ni kero kwa wawekezaji wenye viwanda nchini kwa kile alichokieleza kuwa upatikanaji huo umekuwa ni wa mlolongo wa munda mrefu.
Ameyasema hayo Ofisini jijini Dar es salaam alipokuwa katika kikao cha pamoja kilichohusisha baadhi ya wadau na wamiliki wa viwanda na wenye mashule jijini Dare s salaam ambao wanazalisha maji taka kwa wingi, pamoja na mamlaka ya maji safi na maji taka Jijini Dar es Salaam na Pwani DAWASCO na wamiliki wa miundombinu ya maji safi na maji taka Dar es Salaam DAWASA.
“Kwa wamiliki wa viwanda mliopo hapa nimeshafanya ziara za ukaguzi katika viwanda vyenu halikadhalika na kwa wamiliki wa mashule, nawapa miezi mitatu kwa kila mmoja wenu kuacha kutitirisha maji taka katika mazingira, kuyatibu na kuyaelekekeza katika mfumo wa maji taka wa DAWASCO”.
Hata hivyo, Mpina ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano haitakuwa na uvumilivu katika suala zima la uchafuzi wa mazingira hasa kwa wenye viwanda, na itawachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kuvifunga kabisa viwanda vitakavyo kaidi maagizo ya serikali kwa kuchafua mazingia.