Muft Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir amewataka watanzania na waislamu kwa ujumla kupendeza kwa kuvaa mavazi yanayotengenezwa na kampuni ya mzawa Mussa Bakari ya ‘Islamic Fashion Tanzania’.
Kiongozi huyo waislamu ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizindua kampuni hiyo ya mavazi ya kiislamu Tanzania na kueleza kuwa kwa mujibu wa maandiko ya dini hiyo, wameamrishwa kupendeza kwani Mungu wao ni mzuri na hupenda vitu vizuri.
Amesema kuwa uislamu huambatana na usafi na usafi huo unaanzia kwenye mavazi, hivyo ni vyema waislamu wakaitumia fursa hiyo kwa kununua mavazi kutoka kwenye kampuni hiyo ya mzawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya Islamic Fashion Tanzania, Mussa Bakari amesema kuwa kampuni hiyo imeanza tangu mwaka 2014 ambapo walikuwa wanategemea mavazi hayo kutoka nchi za nje, kutokana na jitihada walizofanya kwasasa wameweza kutengeneza mavazi yao ambapo nusu ya uzalishaji inafanyika Dubai na nusu nyingine atanzania.