Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanza kumfanyia uchunguzi mchoraji wa Nembo ya Taifa, Mzee Francis Maige Kanyasu ambaye kwa mara ya kwanza alikuwa amelazwa katika hospitali ya Amana iliyopo Ilala jijini Dar es salaam .
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya magonjwa ya dharura na ajali Dkt. Juma Mfinanga ambapo amesema kuwa mzee Kanyasu amechukuliwa kutoka hospitali ya Amana ambako alikuwa amelazwa kwaajili ya kupatiwa matibabu ya awali.
“Tumemchukua kutoka hospitali ya Amana baada ya kupata habari zake kwenye vyombo vya habari kuwa hali yake kiafya sio nzuri hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Lawrence Museru akatuagiza tumfuate ili apatiwe matibabu hapa Muhimbili” Amesema Dk. Juma.
Hata hivyo, ameongeza kuwa hospitali ya Amana imemfanyia uchunguzi wa awali kisha kueleza tatizo lake kubwa linalomsumbua kuwa ni kukosa nguvu na kushindwa kutembea hivyo wamemchukua na kumpeleka Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.