Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) katika msimu huu wa maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya sabasaba jijini Dar es salaam limekuja na bidhaa mbili kama ofa kwa watanzania ambazo zitasaidia katika kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza na Dar24Media, Afisa Mawasiliano wa Shirika hilo , Abel Ngapemba amesema kuwa shirika hilo linatambua kuwa nchi yetu imejikita zaidi katika suala la kilimo na watu wengi wanatumia jembe la mkono hali inayopelekea uzalishaji uwe kwa uchache, hivyo katika kukuza kilimo na kuongeza uzalishaji wameamua kuja na bidhaa ya trekta ambazo zitauzwa kwa gharama nafuu kabisa lengo likiwa ni kuendeleza uchumi wa nchi ili kuendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
”Hivyo tumekuja kutoa ofa ya matrekta ambapo mtu analipa malipo ya awali ya milioni 3 tunamwandikia mkataba akishaweka hizo fedha tunamkabidhi trekta na tunamuwekea malipo kidogo ambayo atakuwa analipa ndani ya kipindi cha miaka mitatu” amesema Ngapema
Aidha, amesema kuwa Trekta hizo zina thamani ya milioni 45, lakini NDC wameamua kuwawezesha wakulima kuzichukua kwa kianzio cha milioni 3.
”Trekta ambazo tunatoa sisi thamani yake ni milioni 45, lakini sisi tunakwambia tupatie milioni 3 tu tunakupa trekta hata bajaji huwezi kupata kwa bei hiyo, ni rahisi mno na haina masharti wala riba, sababu lengo letu ni kuwa na maeneo mengi ya nchi yanayolimwa” ameongeza Ngapemba.
Mbali na bidhaa hiyo ya trekta amesema kuwa wamekuja na bidhaa nyingine ambayo ni dawa zinazosaidia kuuwa viluilui wa mbu dawa ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na malaria pamoja na magonjwa mengine yanayotokana na mbu kama vile Dengue, na kama itatumiwa vizuri kwa kuzingatia masharti Ngapemba amesema ndani ya miaka mitatu itasaidia kwa kiasi kikubwa sana kuondoa mbu wa aina yeyote katika makazi ya watu.
Pia ameongeza kuwa lengo kubwa la dawa hiyo ni kuua mazalia ya mbu, hivyo wamekuja na mpango mkakati utakao wawezesha kusambaza dawa hiyo majumbani kwani wamekuwa wakisambaza kwenye halmashauri ambazo zimeathiriwa pakubwa na ugonjwa wa malaria.
Vile vile Napemba amesema kuwa katika maonyesho hayo ya sabasaba, dawa hiyo itauzwa kwa gharama ndogo kabisa ambayo ni shilingi elfu moja kwa kichupa kidogo, hivyo ametoa hamasa kwa Watanzania kutembelea banda lao kuja kuchukua dawa hiyo inayoua viluilui vinavyo sababisha kuzaliwa kwa mbu lengo likiwa ni kuondokana na magonjwa kama vile Dengue na malaria ambayo yanashambulia watu kwa kasi kubwa.
Bofya hapa chini kusikiliza zaidi na kufahamu hasa Shirika la Maendeleo la Taifa NDC.