Taharuki ilitanda angani jana baada ya ndege ya kijeshi ya Umoja wa Kujihami wa nchi za Magharibi (NATO) kuinyemelea ndege iliyombeba waziri wa ulinzi wa Urusi, kabla ya ndege za kijeshi za Urusi kuingilia kati.
Taarifa na picha ya video iliyotolewa na Urusi imeeleza kuwa tukio hilo limetokea katika anga la bahari ndogo ya Baltic kaskazini mashariki mwa bara la Ulaya. Waandishi wa habari waliokuwa wakisafiri na waziri wa ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu wamesema kuwa eneo la tukio hilo humilikiwa kwa pamoja na NATO na Russia.
?Live: Ziara ya Rais Magufuli Mkoani Pwani leo Juni 22, 2017
Kumewahi kuwa na ripoti za kutunishiana misuri kati ya pande hizo mbili katika eneo hilo la anga, lakini hii ni mara ya kwanza kwa tukio linalohusisha kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi.
NATO wamekiri kutokea kwa tukio hilo, kupitia tamko lao kwa njia ya barua pepe lakini wameeleza kuwa kosa lilifanywa na ndege za Urusi ambazo hazikuonesha ishara ya kujitambulisha mapema, hivyo wao wakafanya jitihada za kutaka kuzitambua.
“NATO haikuwa na taarifa kuhusu watu waliokuwa kwenye ndege [ya Urusi], huwa tunafanyia usaili tabia za marubani wa Urusi kwa usalama na weledi,” linasomeka tamko la NATO.
Marekani ambayo ni mwanafamilia kiongozi wa NATO imekuwa katika taharuki za kiusalama na Urusi kwa muda mrefu, hali inayopelekea kila upande kuchukua tahadhari kwa namna inavyowezekana kiusalama.