Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemtaka Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe kuacha kumchafua kwa wananchi.
Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha Bunge, ambapo amemtaka mbunge huyo kuacha tabia ya kumchafua na kuwafanya wananchi kupoteza imani naye kulingana na nafasi yake.
Amesema kuwa ni aibu kwa kiongozi kama huyo kusema uongo mbele ya jamii kwa kutangaza katika mitandao ya kijamii kwamba Spika wa Bunge anaficha baadhi ya nyaraka muhimu zinazo wasilishwa kwake.
”Ndugu yetu Zitto amekuwa muongo, haipendezi kwa mtu mzima, kama hiyo barua ya CAG anadai imeletwa kwangu na kipindi hicho wabunge wote tulikuwa likizo, yeye amejuaje? Anafanya kazi ofisi ya CAG?, barua ya CAG niliipata tarehe 16 nikaipeleka kwenye Kamati ya PAC. hivi kweli ubadhirifu ya Shil. Tri 1.5 nikae kimya? Kama Shil bil. 300 za Escrow tulihangaika wote. sasa hizi taarifa zingine ni kupakana matope ili spika aonekane mtu wa ajabu ajabu hivi. Mheshimiwa Rais alimuuliza CAG kama kuna upotevu wa Sh. Tri 1.5, sote tunakumbuka hapa tulikuwa tunatazama, CAG alikataa,” amesema Spika Ndugai
Hata hivyo, mwanzoni mwa mwaka huu, Zitto aliandika mitandaoni kuwa CAG alikuwa amefanya ukaguzi maalum Hazina, na kubaini wizi au ubadhirifu mkubwa wa Sh. Trilioni 1.5 na ripoti yake kuiwasilisha ofisi za Spika lakini Spika ameikalia ripoti ya CAG, kitu ambacho Ndugai amekipinga na kumtaka mbunge huyo kuacha tabia ya uongo na kumchafua kwa wananchi.