Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage leo Machi 23, 2020 ametangaza tarehe ya kuanza uboreshaji dafrari la mpigakura awamu ya pili pamoja na tarehe ya uwekaji wazi daftari la awali.
“Uboreshaji wa Daftari Awamu ya Pili ambao utaenda sambamba na Uwekaji wazi wa Daftari la Awali utafanyika katika “routes” tatu. ‘Route’ ya kwanza inatarajiwa kuanza tarehe 17 Aprili, 2020,” amesema Jaji Kaijage.
Amebainisha hayo, NEC ilipokutana na wadau wake wakuu (wawakilishi wa vyama vya siasa) ikiwa ni maandalizi ya uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura na uboreshaji wa awamu ya pili wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Ameongeza kwamba katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya pili, vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni kwa muda wa siku nne (4) mfululizo.
Aidha, kuhusu ratiba kamili na maeneo yatakayoanza kutekeleza mazoezi hayo, Jaji Kaijage amesema Tume itatangaza baadae.
Katika hatua nyingine, amesema uchambuzi wa taarifa za zoezi la Uboreshaji kwa Awamu ya Kwanza unaonesha kwamba, Wapiga Kura wapya walioandikishwa ni 7,043,247 sawa na asilimia 30.41 ya wapiga Kura walioandikishwa mwaka 2015, ambapo idadi hiyo imezidi matarajio na makadirio ya awali kwa asilimia 13.41.
“Wapiga Kura waliojitokeza kuboresha taarifa zao ni 3,225,778 ambayo ni sawa na asilimia 13.93 ya wapiga Kura walioandikishwa mwaka 2015. Aidha, idadi ya Wapiga Kura 16,707 sawa na asilimia 0.07 ya wapiga Kura walioandikishwa mwaka 2015, waliondolewa kwenye daftari kwa sababu wamefariki na wengine kupoteza sifa,” ameeleza Jaji Kaijage.
Jaji Kaijage amesema jumla ya Wapiga Kura waliopo katika Daftari la Awali kwa sasa ni 30,187,987, na kufafanua kwamba idadi hii inaweza kubadilika baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki na uchakataji wa taarifa za wapiga Kura endapo watabainika waliojiandikisha zaidi ya mara moja…, Bofya hapa kutazama