Baraza la Usimamizi wa Mazingira Taifa (NEMC) limepanga mikakati ya kutoa elimu ya utunzaji mazingira kwa wachimbaji wa madini hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo alipokuwa akizungumza na Dar24Media kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya madini, ambapo amesema kuwa sekta ya madini imekuwa ikiongoza kwa uchafuzi wa mazingira na ufyekaji miti.
Amesema kuwa kama wachimbaji wa madini wakielimishwa namna bora ya uchimbaji hawataweza kuharibu mazingira kama ilivyo kwa sasa.
“Niseme tu kwamba tuna mikakati ya kutoa elimu kwa hawa wachimbaji wa madini, kama unavyoelewa popote pale kwenye machimbo mara nyingi huwa kuna uharibifu mkubwa wa mazingira,”amesema Dkt. Gwamaka
Aidha, amesema kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kutunza mazingira kwani yanafaida kubwa kwa viumbe hai na shughuli nzima za maendeleo ya binadamu.
Hata hivyo, katika mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili uliwakutanisha wachimbaji wadogo wadogo wa madini, wafanyabiasha na wadau wa sekta ya madini nchini.