Watanzania wametakiwa kuwafichua watu wanaoendelea na utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa pombe aina ya viroba ambazo zimesitishwa hapa nchini kuanzia Machi 1, mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Afya wa Manispaa ya Kinondoni, John Kijumbe wakati wa operesheni ya kuondoa viroba inayoendelea jijini Dar es salaam.
“Pombe ya Viroba imeleta madhara makubwa kwa jamii hasa vijana ambao wengi wao ni waendesha pikipiki (bodaboda) ambapo wamesababisha ajali nyingi nchini kutokana na matumizi ya kilevi hicho,” amesema Kijumbe.
Amesema kuwa kuwa, kama watanzania hawatawafichua wale wanaoendelea na utengenezaji na usambazaji wa viroba vijana wataendelea kuathirika na kuangamia kwa ajali za bodaboda ambazo kwa sasa zimekuwa nyingi .
Aidha amesema kuwa, operesheni hiyo imewezesha kukamatwa kwa tani zaidi ya 400 za viroba katika maghala mbalimbali Jijini Dar es salaam na wamiliki wameagizwa kutosambaza pombe hizo mpaka hapo Serikali itakapotoa agizo la namna ya kuteketeza.
Kijumbe amesema kuwa, Serikali haizuii pombe kali bali imepiga marufuku matumizi ya vifungashio vya plastiki ambavyo vimekuwa vikifungwa kati ya miligramu 50 hadi 100 ambavyo vimepelekea kuuzwa kwa gharama nafuu na bila mpangilio hivyo kuathiri nguvu kazi ya Taifa.
Kwa upande wake Arrison Kileo mmiliki wa duka la Judith na Janet lililoko kinondoni Hananasifu amesema kuwa, ana akiba ya katoni 100 za pombe za viroba aina ya Kiroba Original na katoni 50 za viroba vya konyagi.
Amesema kuwa, amejitahidi kuuza mpaka kufikia tarehe ya mwisho iliyotangazwa na Serikali lakini bado mzigo uliobaki ni mkubwa. Hivyo ameiomba Serikali kuongeza muda ili kumaliza akiba ambayo imebaki kwani pombe hizo wamenunua kwa kufata sheria zote ikiwemo kulipa kodi.
Operesheni hiyo inayoendelea Jijini Dar es Salaam ilianza rasmi Machi 01, mwaka huu ambapo kumekuwepo na changamoto mbalimbali kama vile wahusika wa viwanda na maduka kufunga viwanda au maduka yao ili wasikaguliwe.