Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa amesikitishwa na hatua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kurudia tena neno ‘Udhaifu‘ kwa Bunge alipotoa taarifa yake hivi karibuni.

Spika Ndugai amesema hayo leo Aprili 14, 2019 ambapo amemshauri Prof. Assad akamwone Rais Magufuli ili mzozo wake na Bunge uishe.

“Zipo njia za kumaliza mambo kama haya, mojawapo aende kwa Rais akajieleze kwamba mimi nimepima nimeona nimekosea hapa na pale. Maana Rais ni sehemu yetu sisi (Bunge) hatuwezi kupitisha sheria bila yeye kupitisha mkono wake,” alisema Ndugai.

Ameongeza kuwa hata bajeti inayojadiliwa na Bunge lazima ipitishwe na Rais. Amesema kwa kuwa Bunge limeshapitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Mussa Assad alitakiwa ajiuzulu.

“Kwa kuwa Bunge likishaaamua kuwa halifanyi kazi na mtu, ni uamuzi halali. Katika nchi zote Bunge likishakosa imani na wewe unajiuzulu,” amesema.

Kauli ya Spika inakuja wakati tayari Bunge limeshapitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Assad bali ofisi ya CAG.

“Sasa hatumfundishi kazi Mussa Assad, anampa wakati mgumu Rais tu. Tutafanya kazi na ofisi ya wananchi.”

Spika Ndugai amemsifu Profesa Assad kwa ujasiri wake huku akiufananisha na ujasiri wa mbwa kumtukana mtu anayemlisha. “Unatukana hadi mkono unaokulisha, inahitaji ujasiri na jamaa ana ujasiri. Ila ni ujasiri ule wa mbwa anayemtukana anayemlisha,” amesema.

Aidha, Spika Ndugai amesema hana chuki binafsi na Assad bali tatizo ni lugha tu aliyotumia ya kuliita Bunge dhaifu.
 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Aprili 15, 2019
Tanzania kupokea trilioni 4 kutoka benki ya Dunia