Genge la watu wenye silaha wamevamia na kulazimisha kuingia katika eneo la upigaji picha za video na kuwabaka Wasichana waigizaji wanane, waliokuwa wanajiandaa kuigiza filamu ya muziki nchini Afrika Kusini.
Waziri wa Polisi nchini humo, Bheki Cele amesema tayari wamewakamata washukiwa watatu kati ya 20 kutokana na shambulio hilo la Julai 28, 2022, lililotokea eneo la Krugersdorp, mji mdogo uliopo eneo la magharibi mwa jiji la Johannesburg.
Genge hilo liliwashambulia wafanyakazi na kuwarusha walipokuwa wakishusha vifaa na kuandaa seti za kupiga picha za Video, na kisha kuwatishia kwa silaha walizokuwa nazo na kutekeleza azma yao ya ubakaji.
Wanawake hao wanaodaiwa kufanyiwa vitendo hivyo, walikuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 35, ambapo Waziri huyo wa Polisi Cele amesema mwanamke mmoja alibakwa na wanaume 10 na mwingine wanane.
Amesema, “Hata wanaume nao walivuliwa nguo na kuibiwa vitu vyao vya kibinafsi, na inaonekana ni raia wa kigeni, lakini kimsingi tukio hili ni zama za zama, na lazima tuwatafute wakumbane na vyombo vya sheria.”
Rais wa Africa Kusini, Cyril Ramaphosa amewambia waandishiwa Habari kuwa amemuamuru Waziri wa Polisi kuhakikisha wahusika hao wanakamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Vitendo vya ubakaji nchini Afrika Kusini vimekuwa haviripotiwi mara kwa mara, lakini kwa wastani uhalifu mmoja mmoja kama huo, huripotiwa kwa Polisi kila baada ya dakika 12 katika maeneo tofauti nchini humo.