Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim wanatarajiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu (Ubungo Flyover) eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam Machi 20 mwaka huu.
Hayo yamsemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda alipokuwa akizungumza waandishi wa habari, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo utagharimu takribani shilingi bilioni 188.71 ambapo una lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Morogoro, Nelson Mandela na Sam Nujoma.
“Mradi huo ni sehemu ya uboreshaji usafiri Jijini Dar es Salaam yaani (Dar es salaam Urban Transport Improvement Project), utakaogharimiwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia na mchango wa Serikali ya Tanzania,”amesema Makonda.
Hata hivyo, Makonda amesema kuwa, mradi huo utahusisha pia awamu ya tatu na ya nne ya ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (Bus Rapid Transit- BRT), katika barabara ya Nyerere kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam hadi Gongo la mboto na barabara ya Bagamoyo kutoka katikati ya jiji hadi Tegeta.