Cristiano Ronaldo jana alipeleka kilio kizito Wales na sherehe isiyo na kifani kwa taifa lake la Ureno baada ya kufungua uzio wa mauaji katika nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya.

Katika mechi hiyo ilicyochezwa jana usiku, Ronaldo alifanikiwa kupiga kichwa cha ufundi kilichotikisa nyavu za Wales kwa mara ya kwanza kabla ya nyongeza iliyofanywa na Nani hivyo kuyafanya matokeo kuwa 2-0 na kuipa tiketi Ureno kuingia fainali.

Hii inakuwa fainali ya kwanza ya Ronaldo akiwa na timu hiyo ya Taifa. Rekodi hii mpya ya Ronaldo inaweza kuwa chanzo cha kumfanya asifikirie kabisa kuikacha timu yake ya Taifa kama alivyofanya mshindani wake mkubwa, Lionel Messi baada ya kukatishwa tamaa kwa kushindwa kukibeba kikombe cha ‘CopaAmerica’. Messi alitangaza kuachana na timu yake ya Taifa baada ya kupokea kipigo cha 4-2 kutoka kwa Chile, na kuwafanya waishie kuliangalia Kombe mikononi mwa Chile.

Mpinzani wa Ureno katika fainali atafahamika leo usiku katika mechi ya kukata na shoka kati ya Ujerumani na Ufaransa.

Baada ya kushindwa kuwamudu Ureno, Gareth Bale alisema kuwa ingawa wamekatishwa tamaa na matokeo hayo, wanapaswa kujipongeza kwa kuwa walifanya kila jitihada.

“Tunapenda kuwashukuru mashabiki, ambao wamekuwa na sapoti ya ajabu. Tulijaribu kadiri tuwezavyo lakini tunaomba radhi hatukuweza kuingia fainali,” alisema na kuongeza kuwa hawana majuto kutokana na mechi hiyo bali wanafurahia mafanikio waliyoyapata kufika hapo.

Video: Taifa letu kwa sasa linahitaji Uongozi wenye kuona mbali - Majaliwa
Video: Hii hapa Helikopta ya Mtanzania Adam iliyozinduliwa