Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali haitahusika na ulipaji wa deni la fedha za Ushirika na badala yake kila aliyekula fedha hizo atazilipa mwenyewe.
Majaliwa amesema hayo leo Julai 10, 2017 wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Liwale katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa wilaya.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika na ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi, amesema Serikali haiwezi kukubali Ushirika ukafa nchini kwa ajili ya watu wachache wasiokuwa waaminifu.
Awali, Waziri Mkuu alizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale katika Ukumbi wa Tengeneza, ambapo amewataka Watumishi wa Umma Nchini kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma kwa Wananchi.Amesema Watumishi wanawajibu wa kuwahudumia Wananchi bila ya kutengeneza mazingira ya kuomba rushwa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Lazima Wananchi waone na wanufaike na kazi inayofanywa na Serikali yao, hivyo ni wajibu wa Watumishi kuwatumikia Wananchi popote walipo na si kukaa maofisini.”