Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa Kanda ya Mtwara imewahukumu watu watatu wakiwemo raia wawili wa kigeni na mtanzania mmoja kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja au kulipa faini ya shilingi bilioni 1 baada ya kukamatwa wakifanya uvuvi haramu katika ukanda wa Bahari Kuu Januari mwaka huu.
Watu hao walikamatwa katika ‘Operesheni MATT’ iliyokuwa inaendeshwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola katika Meli ya Buah Naga 1 ya nchini Malaysia wakiwa na kilo 90 za mapezi ya papa bila kuwa na miili yake kinyume cha Sheria kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara na kutakiwa kulipa faini ya milioni 770 ambapo walikwenda mahakamani kupinga adhabu hiyo.
Akizungumzia hukumu hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema tukio hilo ni ushindi mkubwa kwa Taifa la Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli imejidhatiti kulinda rasilimali zake zikiwemo za uvuvi.
Mpina amesema adhabu iliyotolewa na Mahakama Kuu ni kubwa na stahiki kwa washtakiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi yetu na kwamba ulinzi wa rasilimali zilizopo baharini, maziwa, mabwawa, na mito ni jambo muhimu.