Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa shilingi bilioni 1.4 kati ya shilingi bilioni 1.8 zilizotengwa katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya uendelezwaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Akizungumza hayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipotembelea eneo la mtaa wa Wikichi inapojengwa hospitali hiyo akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Njombe, amesema ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020 ya kuwa na zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya katika kila kata, hospitali katika wilaya na hospitali za rufaa kwa kila mkoa.
Amesema lengo la ujenzi wa hospitali hiyo ni kuhakikisha mwananchi anaanza kupata huduma za afya katika eneo lake na anapokuwa na tatizo kubwa ndipo atakwenda hospitali ya wilaya na kisha hospitali ya rufaa ya mkoa.
“Hospitali hii ikikamilika itawapunguzia wananchi gharama za kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma za rufaa. Sasa hakutakuwa na sababu ya kwenda Iringa, Mbeya wala Ruvuma huduma zote zitakuwa zinapatikana hapa hapa Njombe,” amesema.
Amesema kuwa Rais Dkt. John Magufuli ameahidi kuwahudumia na kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali uwezo wao, itikadi zao za kidini na kisiasa na hapa ndiyo maana ya ahadi hiyo ya Serikali ya kuwahudumia. Watu wote watakuja kutibiwa Hospitalini hapo.
Akitoa taarifa ya ujenzi mradi wa hospitali hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Bw Jackson Saitabau amesema kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo kutawapunguzia wananchi gharama kubwa za kufuata huduma za rufaa katika mikoa ya jirani.
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza katika eneo hilo lenye ukubwa wa takribani ekari 70 katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, ambapo kiasi cha sh. 953.705 zilitengwa kati yake sh. milioni 236.575 zilitumika kwa ajili ya ulipaji wa fidia.
“Hospitali hii inajengwa kwa awamu na tulianza na jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambapo gharama za mradi ni sh. bilioni 3.2 huku gharama za mtaalamu mshauri ni sh. milioni 114.160. Mradi ulianza Julai 23, 2016 na unatarajiwa kukamilika Januari 26, 2018,” amesema.