Kufuatia taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikieleza kuwepo kwa mchele wa plastiki, Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) imezungumza kuhusu taarifa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 19, 2017 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hiiti Sillo amesema mamlaka hiyo imefanya uchunguzi na hadi sasa haijathibitisha kuwepo kwa mchele huo nchini kama ambavyo taarifa zimeenezwa.
“Sisi Mamlaka ya Chakula na Dawa tumepata taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii zikizagaa kila sehemu, lakini tunafanya uchunguzi wetu nchi nzima ili tuweze kubaini wapi hasa ulipo mchele huo, hivyo nawaasa wananchi kutoa taarifa pindi tu watakapo uona,” amesema Sillo.