Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, (TFS) imeandaa ziara maalum ya kitalii inayotarajiwa kufanyika kuanzia Tarehe 12  hadi 14 julai mwaka huu kuelekea Lushoto mkoani Tanga kwenye hifadhi ya msitu asilia wa Magamba.

Safari hiyo inatarajiwa kuanzia katika viwanja vya sabasaba ambapo watu watakaojitokeza kwenye ziara hiyo ya kitalii watapata nafasi ya kuona vivutio mbalimbali vya utalii katika msitu asilia wa Magamba.

Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amewataka na kuwahamasisha watanzania kujitokeza kwa wingi katika ziara hiyo ili kufika katika hifadhi ya Magamba na kuwa mabalozi wazuri wa utalii wa ndani.

”TFS, Wakala wa Misitu wanahamasisha utalii katika misitu ya asili, kama mmefuatilia tunao msitu wa Magoroto, Amani, Magamba haya ni maeneo ambayo tunaenda kukutana na utalii wa ndani wa asili, Tarehe 12 mwezi huu TFS wameandaa safari ya kwenda Magamba kama utalii wa ndani, naomba watanzania wajitokeze kwa wingi” amesema Naibu Waziri, Constantine Kanyasu.

Aidha TFS inafanya jitihada nyingi kuhakikisha hifadhi hiyo inajulikana na inatembelewa na watu wengi ndani na nje ya nchi na baadhi ya jitihada ambazo zimeanyika kuendelea kuutambulisha vyema msitu huo ni pamoja na kutumia wasanii wa muziki wa bongo fleva katika kuutangaza msitu wa Magamba.

Moja ya wasanii waliofika na kuutangaza vyema msitu huo ni Linah na Amini ambao walipewa nafasi ya kufanya video ya wimbo wao mpya wa ‘Nimenasa’ uliofanyika kwenye hifadhi ya msitu wa Magamba.

Kufuatia ziara hiyo TFS inawaomba watanzania kutembelea banda la Maliasili na Utalii lililopo sabasaba ili kupata taarifa zaidi kuhusiana na ziara hiyo ya kiutalii ya kuelekea hifadhi ya msitu wa asili wa Magamba.

Hifadhi ya Magamba anapatikana mkoani Tanga, wilaya ya Lushoto, ni hifadhi ya msitu asilia wenye utajiri wa vivutio na hali ya hewa nzuri.

Sikiliza hapa chini.

 

Video: Naibu Waziri atembelea banda la Maliasili na Utalii | Ataja Magoroto, Magamba | Fursa kwa Watanzania
TTCL yaimarisha huduma zake, yavuna wateja lukuki