Pambano kali kati ya mabondia waliotambiana kwa muda mrefu, Keith ‘One Time’ Thurman ambaye hajawahi kushindwa akiwa ulingoni mara 27 dhidi ya mbabe Shawn Porter ambaye rekodi yake sasa inaonesha aliwahi kushindwa mara mbili kati ya mapambano 26, linatajwa kuwa ndilo pambano lililowavutia watazamaji wengi zaidi  mwaka huu.

Pambano hilo lililofanyika Juni 25 mwaka huu katika ukumbi wa Barclays Center, New York Marekani na kuhudhuriwa na zaidi ya mashabiki 12,000, limetajwa kuivunja rekodi ya watazamaji wengi zaidi wa TV kulitazama baada ya ile iliyoachwa na pambano kati ya Muhammad Ali na Leon Spinks, Februari mwaka 1978.

Pambano hilo lililomalizika kwa majaji watatu wote kumpa ushindi Thurman kwa 155 – 113, liligeuka kuwa la utata baada ya mashabiki wengi kuyapinga matokeo hayo na kuzomea kwa nguvu huku Shawn Porter naye akionesha wazi kutoridhishwa na uamuzi huo.

Utata uliongezeka zaidi baada ya USA Today Sports kutoa matokeo tofauti yanayoonesha sare ya 114-114.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Thurman alimsifia Porter kwa kuwa mpambanaji mzuri akidai kuwa aliweza kumshinda kutokana na kuwa na mbinu nzuri zaidi ya kujilinda.

“Kuzuia ndio ufunguo wa ushindi. Alirusha masumbwi mengi na kuwafanya majaji wapate ugumu kumuandikia alama. Mimi niliuwa na uwezo wa kupachika masumbwi yanayoonekana, kwa ufanisi na naamini hicho ndicho kilicholeta utofauti leo,” alisema Thurman.

Naye Porter hakuonesha kulalamika moja kwa moja ingawa alidai kuwa anaamini alishinda na akaomba warudiane akiahidi kumnyang’anya mkanda.

Chadema wakusanyika Dodoma ‘kusaidia Polisi kuzuia mkutano Mkuu wa CCM’
Facebook 'wampiga tofali' mwanamke anayeitwa ‘Isis’, alalama