Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Tanzania, Augustino Lyatonga Mrema ameonyesha kushangazwa na ujasiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli wa kuchukua hatua mbalimbali na maamuzi yenye tija kwa Taifa.
Amesema kuwa haijawahi kutokea kuwa na rais mwenye ujasiri kama Dkt. Magufuli hivyo amewaasa wananchi kwa ujumla kuunga mkono jitihada anazozifanya kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Ameyasema hayo Jijini Dar es salaam alipohudhuria ibaada katika Kanisa la Siloam lililopo Mbezi, Mrema amesema kuwa rais wa sasa ni mfano wa kuigwa na viongozi wote hivyo amewaomba wananchi kuendelea kumuombea ili aweze kutimiza malengo yake ya Tanzania ya viwanda.
“Watanzania tumepata rais ambaye atatufikisha kwenye hatua nzuri ya maendeleo, kwani hata mimi nilikuwa kiongozi mkubwa lakini sikuweza kuyafikia anayoyafanya yeye kwa sasa,”amesema Mrema.
Hata hivyo, Mrema alihudhuria ibaada hiyo kwaajili ya kuombewa ili afya yake iweze kuimarika huku akisisitiza ataendelea kufanya kazi kwa juhudi zote.