Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Warrace Karia amewataka waandishi wa habari kuacha kufuatilia suala zima la mdhamini wa ligi ya Tanzania kwani kufanya hivyo wanaweza kuharibu mazungumzo yanayoendelea.
Ameyasema hayo jijini Dar es salam wakati wa mkutano wake na Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ambapo amewataka waandishi kuwa na subira hivyo wasiendelee kuchokonoa chokonoa.
Amesema kuwa wenyewe kama shirikisho hawawezi kukurupuka kusaini makubaliano na mdhamini asiyekuwa na vigezo, hivyo ni bora ligi isiwe na mdhamini kuliko kuwa na mtu asiyekuwa na faida.
”Kama mnaupenda mpira kaeni kimya, waandishi acheni kuchokonoa chokonoa, mtatuharibia mazungumzo yetu na mazungumzo yetu ni ya siri, hivyo mda ukifika taarifa zote mtapewa,”amesema Karia
Aidha, amesema kuwa suala la mdhamini wa ligi kuu linahitaji kuzungumzwa kwa utulivu, na mda ukifika kila kitu kitawekwa hadharani na kila mmoja atamfahamu mdhamini wa ligi kuu ya Tanzania.