Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kumewezesha kukamatwa kwa wafanyabiashara wakubwa waliokuwa wakitamba kwamba hawawezi kuguswa.
“Sasa hivi dawa zinakamatwa kwelikweli na wale wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliokuwa wakijiita vigogo na kutamba kuwa hawakamatwi na hata wakikamatwa wanaachiwa, wameanza kuikimbia nchi,” amesema.
Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria kwenye Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani yaliyofanyika uwanja wa Gangilonga, mkoani Iringa.
Amesema kuwa, Serikali baada ya kuanzisha Mamlaka hiyo, iliiwezesha kwa kuipatia rasilimali fedha, watendaji na vitendea kazi na tayari mafanikio yameanza kuonekana.
Amesema kila mmoja anapaswa kuliona suala hilo la dawa za kulevya kama jambo hatari kwa mustakabali wa Taifa letu na akasisitiza kuwa watu wasioneane haya katika vita hiyo kwa kuwataja wahusika kwa sababu huuzwa katika mitaa yao na wauzaji wanawafahamu.
“Nawasihi viongozi wa siasa, dini pamoja na vyombo vya habari, tuendelee kukemea kwa nguvu zote matumizi na biashara ya dawa za kulevya,” amesema.
Waziri Mkuu amesema matumizi ya dawa za kulevya yapo zaidi kwenye miji mikubwa hasa ya Dar es Salaam, Arusha, Tanga na Mwanza, pia kasi ya kuenea kwa matumizi hayo kwenye miji midogo nayo ni kubwa hasa katika mikoa ya Iringa, Dodoma na Mbeya na Morogoro.