Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wanaume wote wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wakapime afya zao ili kubaini kama wameambukizwa virusi vya UKIMWI au la.
“Napenda kusisitiza kwa akinababa wote kwamba ukimwi bado upo na wanaume hamuendi kupima, ni wagumu kwenda kupima eti kwa sababu mnawategemea wake zenu waende kupima.”
Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Mwangongo na vijiji vya jirani kwenye mkutano wa hadhara mara baada ya kukagua soko la pamba kwenye kijiji hicho, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
“Unamwambia mama aende kupima virusi vya UKIMWI akija na majibu ukajua hana maambukizi, wewe huku unashangilia kwamba uko salama. Hapana, nendeni mkapime kwa sababu kila mmoja na vyanzo vyake vya kupata maambukizi,” amesisitiza.
Majaliwa pia amewataka wakazi wa wilaya ya Kishapu wajiunge na bima ya afya ili waweze kupata tiba hata wakati hawana fedha.
“Ninawaomba mjiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao utakuwezesha kupata tiba siku ambayo huna hela mfukoni au nyumbani. Pia utakuwa na uhakika wa kupata matibabu bure kwenye zahanati au kituo cha afya chochote kile katika katika wilaya hii,” amesema.