Katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani na kwenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu “Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu”, Kampuni ya DataVision International inayoshughulika na masuala ya TEHAMA, imeungana na wanawake wote ulimwenguni kuadhimisha siku hiyo kwa kuhamasisha wanawake kufanya kazi katika Teknolojia ya mawasiliano TEHAMA.
Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi wa biashara na mahusiano wa kampuni hiyo, Teddy Qirtu amesema kuwa sekta ya Teknolojia ya Mawasiliano inahitaji sana umakini na wanawake ni watu makini hivyo hawanabudi kuwa na kipaumbele cha kufanya kazi za TEHAMA bila kuwa na hofu ya kushindwa.
“Wanawake ni makini sana na umakini wao unahitajika sana katika masuala ya TEHAMA hawatakiwi kuogopa kusoma masomo ya Sayansi kwani wanayamudu na mchango wao unahitajika sana kwenye sekta ya Teknolojia ya mawasiliano,”amesema Qirtu
Aidha, amesisitiza kuwa wanawake ndio viongozi katika jamii hivyo wanatakiwa kujua mabadiliko ya teknolojia kila siku hasa kwa kujihusisha nayo bila kuogopa kwani hata ambaye hajasoma masomo ya sayansi lakini wanapenda kujua vitu vipya kila siku wanaweza kujihusisha na TEHAMA.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wasichana ambao bado wapo masomoni wajitahidi kusoma masomo ya TEHEMA kwa ufasaha bila kukata tamaa kwani sekta hiyo bado inawahitaji kwa kiwango kikubwa sana katika maeneo mbalimbali ambayo hawatakiwi kuachiwa wanaume pekee.