Serikali imetangaza ajira mpya za watumishi 6,180 wa kada mbalimbali za afya katika Mamlaka za serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amesema ajira hizo ni utekelezaji Ilani ya chama cha mapinduzi pamoja na ahadi ya Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.
Aidha, waombaji wote waliochaguliwa katika ajira hizo wametakiwa kuripoti katika vituo vyao vya kazi ndani ya siku 14 kuanzia sasa na atakayeshindwa nafasi yake itachukuliwa na mtu mwingine.
Jafo amesema ajira hizo zimetokana na kibali kilichoandikwa kwa serikali cha kuajiri watumishi wa kada mbalibali wa sekta ya afya nchini.
Amesema kuwa kibali hicho ni mwendelezo wa kibali cha ajira kwa kada za afya 3,152 kilichotolewa mwezi Juli 2017 kwa lengo la kukabiliana na changamoto za utumishi katika vituo vya afya nchini.