Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Sera, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ameziagiza taasisi za umma na binafsi nchini zinapotoa fedha za kusaidia jamii (CSR), zikumbuke kuna kundi maalum la walemavu nchini ambao nao wanahitaji huduma maalum kama wanavyohitaji wengine.

Waziri Mhagama amesema hayo wakati akipokea mashine maalum za kuandikia kwa wanafunzi wasioona (Braille Machines) kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwenye chuo cha walemavu Yombo jijini Dar es Salaam.

“Tunapoona kwenye shule za msingi wanahitaji madawati, tukumbuke kwamba, wapo wanafunzi kwenye vyuo,  wapo wanafunzi kwenye shule za msingi, ambao ni wenye ulemavu ambao pengine badala ya madawati, wao wanahitaji viti vya kuwaongezea mwendo, au kama tunatoa computer mpakato, tukumbuke kwamba tunazo shule na vyuo watoto wetu, vijana wetu wanasoma wenye ulemavu wangehitaji mashine hizi zenye kuandika nukta nundu ili kuwasaidia wenye ulemavu ili na wao wafaidike na elimu katika nchi yetu ya Tanzania.” Waziri Jenista Mhagama

Amesema kuwa amefarijika kuona maagizo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, yameweza kutekelezwa na taasisi ambayo iko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kusaidia kundi hilo la wenye ulemavu.

“Vifaa nitakavyovikabidhi leo ni maalum kwa wenzetu wasioona na ni vya wanafunzi walioko katika vyuo mbalimbali kwenye nchi yetu siyo hapa Yombo peke yake.” amefafanua.

Pia, aliupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa msaada huo mkubwa na kwamba fedha walizotumia kununua vifaa hivyo ni kuwekeza kwa vijana ili kujiandaa kuwa na utashi na weledi na kujiandaa kuingia kwenye soko la ajira nchini.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Septemba 19, 2018
Video: Polepole afichua siri ya ushindi CCM, amshukia Makonda