Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule awakamate viongozi wa Chama cha Msingi cha Mkombozi kwa upotevu wa dola za marekani 21,000 za chama hicho.
“Wabebe hawa watu, wahoji waseme hiyo fedha iko wapi na jambo la kwanza wailete hiyo fedha ya wakulima. Wakishindwa kurejesha fedha, wawekwe ndani,” amesema.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo Julai 16, 2018 wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Kangeme, kata ya Ulowa katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama ambao alienda kuzindua mpango wa Ushirika Afya na NHIF.
Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya kuwaita viongozi wa chama cha Mkombozi watoke hadharani na kubaini kuwa hakuwepo hata mmoja. Inadaiwa kwamba walitoroka baada ya wananchi kuanza kuzomea.
Kamanda Haule amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwenyekiti, Shilinde Abdallah na mhasibu wa AMCOS hiyo, Kulwa Shinzi pamoja na wajumbe saba wa bodi ya chama hicho.