Waziri wa habari, sanaa, burudani na michezo, Nape Nnauye amesema kuwa hana faida yoyote kuwa Waziri wa Habari kama uhuru wa vyombo vya habari utakuwa unaingiliwa.
Waziri Nape amesema hayo leo Machi 20, 2017 wakati alipotembelea ofisi za Clounds Media Group kufuatia tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kutajwa kuwa amevamia katika ofisi hizo akiwa pamoja na Askari wenye bunduki, ambapo tayari ameunda kamati ya uchunguzi ambayo itatoa majibu ndani ya saa 24 ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kufuatia tukio hilo.
Amesema kuwa ripoti ya kamati hiyo iliyoundwa itawekwa hadharani na pia adhabu itakayochukuliwa kwa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda itatangazwa pia.
“Suala la mtu kwenda kwenye vyombo vya habari na bunduki tumezoea kuliona katika nchi zilizopinduliwa, ila hapa Rais yupo” amesema Waziri Nape
Waziri Nape amesema kuwa amejiridhisha kuwa tukio hilo limetokea lakini sasa lazima kujua chanzo cha tukio hilo, ambapo atatoa nafasi kwa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda kusikilizwa ili kuleta usawa na haki kwani hakumu haitatolewa kwa mtu bila kusikilizwa.
“Tumejirisha kuwa tukio hilo limetokea lakini sasa tunataka kujua kwanini tukio hilo lilitokea” – Waziri Nape
Aidha, Nape amesema kuwa kuhusu suala la Makonda kufukuzwa, suala hilo wataiachia mamlaka husika, amesema ripoti ya uchunguzi wa tukio hilo itakabidhiwa katika mamlaka husika.
Amesema mara tu baada ya ripoti hiyo hatua ziitachukuliwa ili kuonyesha kwamba serikali haipendi kuona uhuru wa vyombo vya habari unaingiliwa
Akizungumzia sakata hilo Mkurugenzi Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi amesema tukio hilo limeiaibisha nchi pamoja na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri wa Habari, na Tasnia nzima ya Habari.
“Nilazima tujiulize, huyu mtu aliyefanya tukio hili ametoa wapi ujasiri huo?” – Regnald Mengi
Mengi amesema kuwa Rais Magufuli na Waziri ni wasikivu na wenye upendo, hivyo anaomba upendo huo uonyeshwe kwa vitendo sasa.
Video: Ruge aweka wazi kuhusu Makonda kuvamia Clouds TV