Kama ni muumini wa maandishi yanayosomeka ‘ushindani unaofanana na uhasama’ kwenye biashara ni mtaji mpya wa biashara husika’, basi utakuwa na imani sawa na Young Killer Msodoki.
Rapa huyo ambaye wimbo wake wa ‘Sinaga Swaga’ umewakwaruza baadhi ya wasanii wenzake akiwakaribisha kwenye majigambo ya kupasukiana, ameimbia Dar24 katika mahojiano maalum hivi karibuni kuwa moja kati ya vitu vinavyoukwamisha muziki wa hip hop nchini ni kukosekana kwa ushindani wa wazi baina ya wasanii, hali aliyodai inaletwa na ushkaji kazini uliojengeka baina yao.
“Wasanii wa hip hop tufanyeni kazi, na urafiki-urafiki wetu huu kwenye kazi utaufanya muziki wa hip hop usifike mbali. Muziki wa waumbaji unafika mbali na unaona sasa hivi akina Diamond wana machupa hadi na akina Ne-Yo kwa sababu muziki wao wana-challenge, urafiki-urafiki wa kipumbavu haupo,” Young Killer aliiambia Dar24.
“Ushikaji ushkaji kwenye kazi yetu ndio unaoharibu. Unakuta Young Killer anaushikaji na Godzilla, Godzilla ana ushkaji sana na Nikki wa Pili, hicho ndicho kinachoharibu. Game sasa inatakiwa kuwa ki-challenge zaidi, alifunguka rapa huyo ambaye ni C.E.O wa Matunzo Zero Unit Entertainment.
Mkali huyo wa michano alifafanua kuwa hali ya kuwepo uhasama wa kikazi huleta changamoto na chachu inayozaa biashara zaidi na kusogeza muziki mbele.
“Inakuwa ni biashara… [kwa mfano] wakisikia kuwa Young Killer ana bifu na Dogo Janja, yaani ikiandaliwa show watu lazima wajae. Ikiandaliwa show ya Young Killer watu lazima wajae kujua atafanyaje, ikiandaliwa show ya Dogo Janja lazima wajae kuona atafanyaje. Kwahiyo huu urafiki-urafiki ndio unafanya hata game yetu inakuwa inapoa,” amesema.
Killer aliongeza kuwa yeye ndiye msanii ambaye amekuwa akiwekewa changamoto ya kuchanwa na kupaniwa na wasanii wapya zaidi ya wasanii wengine lakini huipokea kwa mtazamo chanya na kupambana zaidi. Hivyo, aliwataka wote aliowakwaruza kwenye ‘Sinaga Swaga’ wao pia wajifunze kuipokea kama anavyopokea kutoka kwa wengine.
Katika hatua nyingine, Young Killer alisema kuwa wiki hii ataachia remix ya ‘Sinaga Swaga’ ambayo itakuwa kwenye ujazo wa audio na video.
Endelea kutembelea Dar24.com uwe wa kwanza kuipata.