Vifaranaga 5000 vilivyokamatwa kutoka nchini Kenya vikiingizwa nchini kinyemela vimeteketezwa kwa moto ili kuepusha tishio la kuwepo kwa ugonjwa wa mafua ya ndege.
Vifaranga hivyo vimekamatwa katika eneo la mpakani mwa Kenya na Tanzania, Namanga ambapo baada ya kukamatwa vifaranga wa kuku wa mayai 5000 wenye thamani ya Tsh 11,500,000 na Trei 416 zenye mayai, yenye thamani ya 3,120,000/ kwa pamoja vimeteketezwa kwa moto kwa kuzingatia haki za wanyama (Animal welfare) ambapo kabla ya kuteketezwa mifugo hiyo ililazwa kwa kutumia dawa aina ya Farmaldehyde na kuhakikisha wamekufa kabla ya kuchomwa.
Hata hivyo, Mayai hayo pamoja na vifaranga vimekamatwa vikiingizwa nchini kinyume na sheria, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la chakula (FAO) ya mwezi Desemba ilitoa tahadhari kuwa nchi ya Tanzania pamoja na nchi jirani Kenya na Uganda na nchi nyingine za Afrika ziko hatarini kuambukizwa mafua ya ndege.