Idadi ya watu waliokufa duniani kutokana na janga la virusi vya corona imefika 400,000, huku vifo vikiongezeka kwa kasi katika kitovu cha janga hilo cha Amerika kusini.
Karibu visa milioni 7 vya maambukizi ya COVID-19 vimeripotiwa tangu janga hilo lilipozuka nchini China mwishoni mwa mwaka jana.
Ulimwengu ulichukua hatua za kusitisha shughuli muhimu na kuuathiri uchumi wa dunia. Hata hivyo, hofu ya kuzuka wimbi la pili la ugonjwa huo hatari imeibua wasiwasi mkubwa.
Katika kujaribu kuishi na virusi hivyo kwa muda mrefu, nchi za Ulaya zimelazimika kufungua upya mipaka yake na makampuni, na nchi nyingi barani Asia na Afrika kuanza kurejea taratibu katika maisha ya kawaida.
Umoja wa Ulaya umesema utafungua mipaka yake kwa wasafiri kutoka nje ya kanda hiyo mapema mwezi Julai baada ya mataifa kadhaa ya umoja huo kuanza kuruhusu wageni kutoka mataifa jirani ya Ulaya kuyatembelea.