Tanzania imeongeza kiwango cha upimaji cha ugonjwa wa malaria kutoka asilimia 64 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 99 mwaka 2018 na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa Asilimia 63 kutoka watu 6,737 hadi 2,540.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu katika mkutano wa 20 wa kisera wa wadau wa sekta ya afya uliofanyika Jijini Dodoma Novemba 19, 2019.
Amesema sambamba na hatua hiyo pia Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi mapya ya VVU asilimia 20 kwa watu wazima na asilimia 31.3 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 15 katika mwaka 2010/2018.
“Kiwango cha upimaji malaria kimepanda hadi asilimia 99 na tumepunguza maambukizi ya VVU kwa watu wazima na watoto ila kuhusu kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano nacho kimepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2015 mpaka 31.8 mwaka 2018,” amefafanua Waziri Ummy.
Wakiwa katika kikao hicho wadau wa masuala ya afya wamekubaliana kutekeleza vipaumbele vilivyopitishwa ikiwemo kuboresha utekelezaji wa mikakati ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.
Vipaumbele vingine ni pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za uzazi kwa vijana wadogo, kuboresha utoaji wa huduma za dharura na kushirikiana na wadau kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya.