Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson amewataka vijana kuacha matumizi ya tumbaku, pombe, dawa za kulevya na shisha kwani hupelekea vijana wengi kuwa na tatizo la afya ya akili na kupoteza nguvu kazi ya taifa pamoja na kuendelea kujikinga na maambukizi ya VVU, magonjwa ya ngono na kufanya mazoezi kwa wingi na kula vyakula bora kwa afya ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.

Apson ameyasema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida katika kutamatisha Bonanza la michezo la kuelimisha na kutoa huduma za afya kwa vijana katika manispaa ya Singida na kuipongeza Wizara ya Afya kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kuweza kuwakutanisha vijana na kupatiwa elimu na huduma mbalimbali za upimaji afya ambapo zaidi ya vijana 1553 wamefikiwa.

Amesema, “Vijana ni nguvu kazi ya taifa katika nchi yetu vijana wanategemewa katika maendeleo ya nchi yetu, ili Tanzania iwe taifa lenye nguvu ni wazi inahitajika jitihada kubwa katika kuwekeza katika afya za vijana na elimu, jambo hili litawezesha kuwa na vijana wenye nguvu ya kuwajibika katika maisha yao wenyewe, familia zao na taifa kwa ujumla.”

Naye, Afisa kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana, Jesca Masanja amewataka vijana kutumia vyema elimu ya afya waliyopewa na wataalamu wa afya ili kuweza kutunza afya na kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kuepukana na magonjwa mbalimbali.

Wanaharakati 39 wa upinzani wafunguliwa mashitaka
Changamoto ndoa na mtoto wa Bosi yampa mbinu za kivita