Vijana Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma, wametakiwa kuchangamkia fursa ya mikopo nafuu ya ujenzi wa Vituo vya Mafuta Vijijini, inayotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini – REA.
Wito huo, umetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wakati wa Semina ya Nishati Safi ya kupikia, iliyotolewa na Wataalam wa REA kwa Baraza la Umoja wa Vijana na Umoja wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Wilayani humo.
Amesema, “tuungae mkono Ajenda ya Mhe. Rais ya kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala. Nimekuja na Wataalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wao watatueleza umuhimu wa nishati mbadala, lakini pia watatueleza fursa ambazo zinapatikana, ambazo vijana na wazazi mnaweza kuzitumia.”
Aidha, Naibu Waziri pia amewataka V+ijana na wazazi walioshiriki semina hiyo kuchangamkia fursa ya mikopo nafuu inayotolewa na REA kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini, ambapo amewataka vijana hao na wazazi kuomba mikopo hiyo ili waweze kujenga Vituo vya Mafuta ambavyo pia vitawaangizia kipato.
Akieleza kuhusu fursa ya mikopo nafuu ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini, Mhandisi Kelvin Tarimo kutoka REA, amesema ni ya Mwananchi yeyote anayeishi Vijijini na kwamba mikopo hiyo imekuja kutokana na hali ya upatikanaji wa mafuta wa maeneo hayo kutokuwa salama.
Amesema, fedha zinazotolewa kwenye mkopo huo ni Shilingi 75 Milioni ambazo zinatolewa kwa awamu tatu, ya kwanza na ya pili kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa kituo, na awamu ya tatu ni kwa ajili ya kuagiza mafuta na kuanza biashara na marejesho yake huenda hadi miaka saba.