Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, ameridhishwa na viwango vya wachezaji vijana chini ya umri wa miaka 17 (U-17) kutoka Wilaya ya Temeke na Kigamboni waliojitokeza kwenye majaribio yaliyofanyika jana Jumapili ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam FC imeanza mchakato rasmi wa kuunda kizazi kipya cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, mpango ambao itazunguka mikoa 13 nchi nzima, ambapo kwa kuanzia tayari imefanikiwa kumaliza majaribio ndani ya eneo la Wilaya ya Temeke na Kigamboni, wakijitokeza vijana 423 na kuchaguliwa watano tu.

Legg ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mara baada ya zoezi hilo kukamilika kwa mafanikio makubwa kwenye maeneo hayo mawili, hivi sasa amewakaribisha vijana wa umri huo kutoka Wilaya ya Ilala watakaotakiwa kujitokeza kwa wingi ndani ya Uwanja wa Jakaya Kikwete Park (JMK Park) Jumamosi ijayo Septemba 3 mwaka huu.

Vijana hao watatakiwa kufika kwa ajili ya majaribio hayo kuanzia saa 1.00 asubuhi wakiwa na vyeti vyao vya kuzaliwa na wazazi au walezi wao, ambao watawaongoza na kuwashuhudia wanapoonyesha viwango vyao pamoja na kutoa msaada wowote wa kumwelezea kijana wake pale itakapohitajika.

“Kulikuwa na viwango vizuri leo (jana), tulitarajia kupokea vijana zaidi takribani 500 hapa lakini wamejitokeza 423, lakini tunaamini tutapata vijana zaidi kwa majaribio ya pili Wilaya ya Ilala ndani ya JMK Jumamosi ijayo.

“Viwango vilikuwa vizuri, hususani dakika 45 za mwisho kwenye mechi iliyohusisha vijana 23 tuliowachagua hadi mchujo wa mwisho na hatimaye kupata watano wa mwisho, hatukuweza kuchagua wengi zaidi kwa kuwa tunachagua vijana bora zaidi Tanzania nzima, lakini tumeshuhudia viwango vizuri sana,” alisema.

Kocha huyo raia wa Uingereza, alisema kwa wale walioshindwa kuchaguliwa kwenye mchujo huo wa kwanza Temeke na Kigamboni, atawapa nafasi nyingine ya mwisho kurejea tena kuonyesha vipaji vyao Novemba mwaka huu, kabla hajaendesha mchujo wa mwisho kwa muda wa wiki moja kwa vijana wote aliowachagua kutoka maeneo yote Tanzania.

Majaribio Ilala                                                              

Legg aliyewahi kufanya kazi kwenye kituo cha kukuza na kulea vipaji cha staa wa Wales, Craig Bellamy, kinachoitwa Craig Bellamy Academy kilichopo nchini Sierra Leonne, alisema kuwa anatarajia kupata vijana wengi watakaojitokeza kwenye majaribio ya Wilaya ya Ilala.

“Naamini viwango vinatarajia kuwa kama vya hapa Temeke au bora kabisa kutoka eneo hilo, nawakaribisha sana vijana wa Ilala,” alimalizia Legg.

Azam FC ni moja ya timu zilizotoa vijana wengi chipukizi wanaotamba hivi sasa kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na timu za Taifa nchini, wakiwemo Simon Msuva wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba), Rashid Mandawa (Mwadui).

Walioko timu za Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 ni winga Yohana Mkomola na kipa namba moja wa kikosi hicho, Ramadhan Kabwili, ambao kwa kushirikiana na wenzao wameweza kuitoa Afrika Kusini (Amajimbos) na kungia kwenye mchujo wa mwisho wa kufuzu Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo (Madagascar), ambapo sasa wanasubiria kucheza na Congo Brazzaville.

Moja ya vijana inayoendelea kunufaika nayo kwenye timu ya wakubwa ya Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kiburudisho safi cha Azam Cola, ni kipa namba moja Aishi Manula, mabeki Ismail Gambo ‘Kusi’ na Gadiel Michael, viungo Mudathir Yahya, Abdallah Masoud na mshambuliaji Shaban Idd.

Kinda mwingine Farid Mussa, tayari nyota yake imeanza kung’ara kwani muda wowote kuanzia sasa anatarajia kujiunga na Club Deportivo Tenerife ya Hispania, ambayo kwa sasa inamalizia taratibu za yeye kupata kibali cha kufanya kazi akiwa nchini humo.

Wengine ambao wamepelekwa kwa mkopo kwenye timu mbalimbali Ligi Kuu ni beki Abdallah Kheri (African Lyon), kiungo Bryson Raphael (Ndanda), winga Joseph Kimwaga (Mwadui) na mshambuliaji Kelvin Friday (Mtibwa Sugar).

Kipa Aliyeinyima Ulaji Simba SC Aitwa Taifa Stars
Amtumia mpenzi wake zawadi ya chatu akiwa hai akizuga ni ‘msosi’