Serikali Nchini, itahakikisha inawalinda Vijana kwenye soko la ajira kwa kuhakikisha ajira zao za kwanza kwenye utumishi zinazingatia vigezo vya utaalamu wa kada husika na sio uzoefu kazini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete hii leo Novemba 01, 2023 Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Ngwasi Kamani aliyehoji kigezo cha kutakiwa uzoefu katika kuomba kazi kwa vijana waliohitimu vyuo kuwa ni ubaguzi kwa vijana wanaoanza kuomba ajira.

Amesema, “ajira za Serikali zinatekelezwa kwa kuzingatia sera ya menejimenti na ajira ya mwaka 2008. Kwa mujibu wa aya ya 4 kifungu cha 2 (i) inaelekeza kwamba ajira ya kwanza hususani kwa wale wanaoajiriwa kwa cheo cha kuanzia kwenye miundo ya serikali itafanyika kwa kuzingatia vigezo vya utaalamu bila kujali uzoefu.”

Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.

Kikwete ameongeza kuwa, “isipokuwa kama ajira husika itahitaji kuwa na uzoefu. Suala la uzoefu lipo kwenye madaraja ambayo si ya kuingilia kazini kama nafasi za waandamizi, viongozi au kada ambazo uzoefu ni sifa za msingi kuingia kama vile udereva ambao mtumishi lazima ajue kuendesha gari kwa viwango vilivyowekwa.”

Katika swali la nyongeza, Mbunge Kamani alitaka kujua kauli ya serikali kwa waajiri wa sekta binafsi wanaoendelea kutumia kigezo cha uzoefu kutangaza ajira pamoja na serikali kuwatambua na kuwapa kipaumbele wahitimu wote wanaojitolea kwenye ofisi mbalimbali za umma.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kikwete amesema serikali kupitia kwa ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha waajiri wote wanazingatia vigezo vinavyotakiwa katika soko la ajira huku wakiendelea kutoa maelekezo ya mara kwa mara.

Aidha, Kikwete alikamilisha majibu yake hayo bungeni kwa kusema kwasasa serikali inaendelea kukamilisha sheria na muundo wa utumishi ambao utawatambua vijana wote wanaojitolea ili waweze kuingia kiurahisi katika soko la ajira.

Wafugaji kuweni mabalozi uhifadhi wa Mazingira - Dkt. Jafo
Aishi Manula aipasua Simba SC