Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Vijana wajitambue na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, huku akiwahimiza watu wanaoishi na VVU kuendelea kutumia dawa za ARV kwa usahihi, ili kufubaza VVU na kuimarisha afya zao.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Desemba mosi, 2023 katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Morogoro, mjini Morogoro.
“Wadau wote wekeni kipaumbele katika kundi hili muhimu ili kulinusuru na athari za UKIMWI. Taifa linawategemea, Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za ARV nchini zinapatikana,” amesema Majaliwa.
Aidha, ameitaka Mikoa na Wilaya zote nchini kutekeleza maelekezo ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani na kutoa huduma stahiki kwa wananchi, huku akitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini, siasa na wakimila kutumia majukwaa waliyonayo kuendelea kukemea taarifa za ubaguzi dhidi ya WAVIU na kuhimiza upendo.
“Kila mkoa uandae taarifa ya maadhimisho itakayoainisha huduma mbalimbali za kijamii na kuiwasilisha kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama alisema ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) pamoja na Waziri wa Afya watajipanga kuhakikisha wanawalinda vijana wa Tanzania dhidi ya janga la UKIMWI.