Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais , Muungano na Mazingira, Dkt.Selemani Jafo amewataka Vijana kutoka sehemu mbalimbali Duniani kuinua sauti na kuelezea wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la hasara na uharibifu unaohusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Jafo ameyasema hayo alipofungua Kongamano la tatu la Kimataifa la Viongozi Vijana na Mabadiliko ya tabianchi (GLOBAL YOUTH CLIMATE SUMMIT) lililofanyika jijini Dar es Salaam na kuwataka vijana hao kuwa Mabalozi wa Kampeni ya Nishati safi ya kupikia na Teknolojia, kuendeleza usawa wa kijinsia kwa wanawake wa vijijini na vijana katika nchi zinazoendelea, na kuchukua jukumu la kuhamasisha mabadiliko.
Amesema, “Kongamano hili ni jukwaa la kipekee vijana wenye ujuzi tofauti mnakutana kwa lengo la kuongeza uelewa wenu wa sayansi ya mabadiliko ya tabianchi, kukuza uongozi, na kutengeneza suluhisho zitakalopeleka kuzuia na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.”
Aidha, Dkt. Jaffo pia amewataka washiriki wa konngamano hilo kubadili mtazamo wao kutoka kwenye utayarishaji wa nyaraka kuwa vitendo kwenye ngazi ya jamii, huku akikipongeza Kituo cha Uongozi wa Vijana wa Kimataifa (Global Youth Leadership Center), kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu wa Tanzania (TFS) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa juhudi zao za kuwawezesha vijana na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za uchumi wa kijani na mabadiliko ya tabianchi.