Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama ameeleza kufurahishwa na kasi ya uwekezaji wa wanachama katika kampuni ya JATU PLC na namna inavyowakomboa vijana kuondokana na changamoto za ajira na uchumi.
Waziri Mhagama ametoa pongezi hizo wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 5 ya kampuni hiyo toka ianzishwe mwaka 2016.
Waziri Mhagama amefafanua kuwa, Kampuni ya JATU PLC imekuwa kiuongo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kupitia miundombinu thabiti iliyojiwekea ambayo imejikita katika shughuli za kilimo, viwanda na masoko hivyo zimekuwa ni msaada kwa wanachama kuondokana na umaskini.
“JATU PLC ni kampuni iliyoanzishwa na vijana, nafurahi kuona mmeweza kushiriki katika juhudi hizi za Serikali kwa kuhakikisha mnazalisha malighafi na kuongeza thamani ya Mazao mnayozalisha kupitia Viwanda kwa lengo la kuwa na mnyororo wa kuongeza thamani na kulinda ajira za vijana wetu ili kupitia mnyororo huo wa thamani muweze kutoa ajira nyingi na kujipatia kipato,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha amesema kuwa utafiti wa nguvukazi uliofanyika 2014 ulibainisha asilimia 56 ni vijana hivyo kupitia fursa ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na kampuni ya JATU PLC ni vyema ikatumika kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto ya ajira kwa kuwashiriki katika miradi ambayo itawaletea matokea yenye tija.
Pia ametoa rai kwa vijana wote nchini wahitimu wa vyuo vikuu, vyuo vya kati, Sekondari na hata msingi kujiunga katika vikundi na kusajili Kampuni au vikundi vyao ili waweze kusaidiwa kwa urahisi na waweze kutimiza ndoto zao.