Serikali imetoa wito kwa vijana kote nchini kuchangamkia fursa ya kupata ujuzi wa fani mbalimbali kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Robert Masingiri wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu programu hiyo.
Masingiri amesema kuwa programu hiyo ni muhimu kwa vijana kwani itawawezesha kupata ujuzi na stadi stahiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
“Utekelezaji wa programu hii ni hatua za makusudi za Serikali za kukabiliana na kiwango kidogo cha ujuzi miongoni mwa nguvu kazi ya Taifa.” Alisema Masingiri.
Aidha, ameongeza kuwa kiwango cha ujuzi hakijafikia hatua nzuri ya kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati hivyo Serikali imetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya programu hiyo na utekelezaji wake umeanza mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2020/2021.
Kwa upande wake, Afisa Habari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Ridhiwani Wema amesema kuwa programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali kwa njia ya uanagenzi (apprenticeship) ambapo lengo ni kuwafunza vijana 3000 katika viwanda vya nguo na vijana 1000 katika sekta ya ngozi.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuendelea kukamilisha miongozo ya ukuzaji ujuzi kwa njia mbalimbali itakayowezesha wadau kushiriki katika utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini ili kufikia sera ya kukuza viwanda na kujenga uchumi wa kati