Vijana nchini kote wametakiwa kujua wajibu wao na kujifunza historia ya nchi na viongozi waliojitolea kuleta uhuru, umoja, amani na maendeleo ya watu .
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Kwanza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Dkt. Salim Ahmed Salim.
Amesema kuwa athari za vijana kutojua historia ya nchi na viongozi waliopigania uhuru ni pamoja na kukosa uzalendo na uwajibikaji katika kutekeleza malengo ya Serikali katika kuleta mapinduzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
“Mimi binafsi naipongeza Serikali yetu kwa kuonesha nia njema ya kupunguza au kuondoa changamoto, zinazowakumba vijana wetu. Vijana ni wengi kuliko kundi lolote nchini na hawana uhakika wa maisha yao ya kila siku hivyo wanahitaji kubadilika.”
Hata hivyo, ameongeza kuwa nafasi waliyonayo kama vijana ni kujifunza jinsi viongozi walivyoweza kuweka misingi ya umoja, amani, mshikamano na changamoto zilizowakabili na jinsi walivyoweza kuzitafutia ufumbuzi badala ya kukata tamaa na kuilaumu Serikali kuwa haiwasaidii.