Waziri wa Nishati, January Makamba ametoa ufumbuzi wa changamoto ya muda mrefu ya mgawo wa umeme wa masaa 12 kwa vijiji 20 vilivyopo Wilaya ya Ludewa, ambavyo vimekuwa vikipata umeme kutoka kampuni moja inayoendesha mradi mdogo wa umeme wa maji wa Megawati 1.7.
Kampuni hiyo, inayoundwa na wadau mbalimbali wakiwemo Jumuiya ya Watumia Umeme Lugarawa na Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, imetajwa kuwa na changamoto ya mgawo wa umeme kwa kuwa na waya mdogo wa kusambazia huduma hiyo.
Wananchi hao, wamedai kuwa umeme huo hauwatoshelezi kutokana na shughuli za kiuchumi wanazoziendesha ikiwemo kukamulia mafuta ya alizeti, kukoboa na kusaga nafaka vitu ambavyo vinahitaji uwepo wa umeme wa uhakika.
Akijibu hoja hiyo mbele ya Wananchi wa Kijiji cha Lugarawa, Waziri Makamba amesema, “Serikali kupitia TANESCO imeamua kununua umeme unaozalishwa na kampuni hii baada ya kufanya mazungumzo na wadau wanaohusika pamoja na TANESCO.”
Amesema uamuzi huo umefanyika ili kuwezesha Wananchi kupata umeme wa uhakika kwani kwa sasa katika megawati 1.7 zinazozalishwa zinaotumika ni 0.3 pekee ambapo kampuni hiyo itaingia katika mfumo wa kupata mapato.
Aidha, Waziri Makamba ameongeza kuwa, “Wataalam wa TANESCO watafika hapa Lugarawa tarehe 7 Agosti 2022 ili kufanya tathmini ya Miundombinu ya Usafirishaji umeme pamoja na kusaini mikataba ya makubaliano hayo.”
Amesema, “Inategemewa kuwa ifikapo mwezi wa Pili mwaka 2023 wananchi wote wa Ludewa mtakuwa mmeshaanza kupata umeme wa uhakika.”
Mradi huo wenye wateja 3200, kwa sasa umeleta manufaa mbalimbali kwa Wananchi wa Kijiji hicho ikiwemo kutoa huduma ya umeme katika vituo vya afya, shule tano za Sekondari, shule 19 za msingi na kituo kimoja cha kulelea watoto yatima.
Utekekelezaji wa Mradi wa umeme huo wa Madope umefanikiwa baada ya kuwezeshwa na wadau mbalimbali ikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), uliotoa shilingi 4.5 Bilioni za kuendeleza mradi huo.