Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kufuatia matokeo ya Tathimini ya Hali ya Upatikanaji wa Maji Vijijini katika Vijiji 12,314, iliyofanywa na Wizara ya Maji na kupelekea kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini-RUWASA, Wizara imefanikiwa kupeleka maji katika vijiji 9,671 na vijiji 2,643 vilivyobaki vitakamilika ndani ya miaka miwili ijayo.
Akizungumzia utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Maji wa chanzo cha Ziwa Victoria, Aweso amemuhakikishia Rais mradi huo unatekelezwa kwa kasi na kesho Oktona 17, 2023 ataenda kuzindua Mradi wa maji wa chanzo hicho wa Tinde-Shelui.
Amesema Mradi Mkubwa wa Maji wa Miji 28 unaendelea kutekelezwa, ikiwa ni sehemu ya matunda ya ziara yake nchini India na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutaondoa kabisa adha ya maji kwa maeneo hayo.
Waziri Aweso ameshiriki Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mkoa wa Singida katika Uwanja wa Bombadia, ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku tatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Mkoani Singida.